Raia wa Kongo wenye asili ya kitutsi wamekuwa wakijiandikisha katika zoezi la kupiga kura huku wakilindwa na Polisi wenye silaha mjini Nyangezi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kutokana na hofu za uwepo wa ghasia na uvumi wa kuenguliwa katika uchaguzi ujao.
Raia hao wamedai wamekuwa wakishambuliwa kwa mawe na fimbo na makundi ya Vijana wa maeneo hayo wanapoenda kujiandikisha katika daftari la upigaji kura, kitendo abacho wamesema kinawapa hofu ya kushiriki zoezi hilo siku husika.
Mmoja wa watu waliojeruhiwa, Philippe Ruhara amesema, “walikuwa wakisema nenda kwenu huku wakirusha mawe na kuchapa watu kwa fimbo na wanatutenga wakidai sisi ni Watutsi tunaoishi katika jimbo la Kivu Kusini tukijulikana kama Banyamulenge.
Aidha, Ruhara ameongeza kuwa, watu wengi katika jumuiya yake wamekuwa wakipokea vipeperushi vinavyowaonya kutopiga kura, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya chuki inayoshuhudia katika makundi ya vijana wa kiume waliokusanyika katika vituo vya uandikishaji kuwazuia wapiga kura wenye asili ya Kitutsi.