Watu wawili wanaosakwa na Serikali ya Uingereza kwa tuhuma za kuiba zaidi ya shilingi bilioni 330 kupitia kodi, wamebainika kuishi Tanzania kwa utulivu wakitumbua ukwasi wao na kumiliki kampuni.

Kwa mujibu wa gazeti la daily records, watuhumiwa hao ambao ni mtu na baba yake, Geoffrey Johnson (baba) na Gareth Geoffrey (mwana), walihukumiwa bila kuwepo mahakamani nchini Uingereza huku wakiendelea kutafutwa.

Wiki iliyopita, Jaji aliwahukumu wawili hao kulipa deni lao la mabilioni au kutumikia kifungo cha miaka 14 jela kila mmoja. Watu hao wanatafutwa baada ya kukimbia kesi hiyo mwaka 2013 na mwaka 2014.

Chombo kimoja cha habari cha Scotland kimeeleza kuwa Geoffrey na Gareth wanadaiwa kumiliki kampuni waliyoipa jina la Jonson International Group iliyoko Kipawa jijini Dar es Salaam ikiwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 125. Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekaririwa wakisema kuwa kampuni yao iko katika hali ngumu kifedha.

Imeelezwa kuwa wawili hao wanaishi mkoani Iringa hivi sasa na kwamba walihama kutoka Dar es Salaam baada kampuni yao kuanza kuyumba na kushindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wao.

Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha ‘Interpol’ nchini, Gustav Babile alimwambia mwandishi wa habari wa The Citizen kuwa ofisi yake bado haijapata taarifa rasmi kutoka Uingereza kuhusu watu hao.

“Hatuna taarifa hiyo na tunayasikia hayo sasa hivi kutoka kwako. Tutaujulisha umma kama kutakuwa na taarifa kama hizo,” alisema.

Kadhalika, Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Peter Kakamba alisema kuwa Jeshi hilo halijapata taarifa ya watu hao.

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walieleza kuwa wamiliki hao walikuwa wakiishi maisha ya anasa na kumiliki magari ya kifahari.

 

Tajiri Wa Kiarabu Kuiongoza African Lyon
Antonio Conte Ajivisha Kitanzi Kilichomnyonga Mourinho