Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa amewataka wahitimu wanaohitaji kutuma maombi kwa ajili ya kujiunga na Vyuo vya Elimu ya Juu, kuzingatia umakini katika uombaji kwa sababu hakuna kubahatisha.
Ameyasema hayo ikiwa ni si chache tu tangu Baraza la Mitihani la Taifa, kutangaza matokeo ya kidato cha sita, ambapo amesisitiza kuwa wanaoomba wanapaswa kuomba kupitia tovuti za Vyuo husika, na yatafanyika kwa njia ya kielektroniki.
“Wanatakiwa kusoma miongozo inayotakiwa, hivyo waombaji wasome kwa umakini kwani hapa hakuna kubahatisha, na kwa yeyote ambaye hajatimiza sifa basi asijaribu kuomba kwani hatopata, hivyo waombaji waingie katika vyuo husika,” amesema Prof. Kihampa.
Dirisha la udahili litafunguliwa rasmi siku ya Julai 15, 2019, ambapo waombaji wote na wazazi kwa ujumla, wametahadharishwa kujiepusha na wale watu wanaojiita mawakala, hivyo wanapaswa kuwasiliana na chuo husika kwa ufafanuzi zaidi.