Maafisa wa serikali nchini Cameroon, wanasema takriban Wanawake 30 wametekwa nyara na wanamgambo wanaopigania kujitenga na wenzao wanaozungumza kiingereza, huku wakidai utekaji nyara huo ulitokana na wanawake hao kupinga ushuru haramu wanaotozwa na wanaharakati hao.
Afisa wa ngazi ya juu katika eneo hilo, Emil Mooh amesema wanawake hao walichukuliwa katika kijiji cha Babanki, karibu na mpaka na Nigeria na kusema wengi wa wanawake hao waliteswa na wengine kupigwa na bunduki na mapanga.
Amesema, wapiganaji hao walikuwa wanakusanya malipo ya kila mwezi kutoka kwa watoto, wanawake na wanaume, kwa kuwatoza wanandoa ushuru kabla ya kuoana, na kuzilazimisha familia kulipa dola 1,000, ili kuwazika jamaa zao.
Cameroon imekumbwa na mapigano tangu wanaharakati wa eneo linalozungumzwa Kiingereza kuanzisha uasi mwaka wa 2017 na waasi hao wametangaza lengo la kujitenga na eneo lenye wakaazi wengi wanaozungumza Kifaransa na kutengeneza mkoa huru, wa wanaozungumza Kiingereza.