Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka bandia 240 za serikali ambazo wamekuwa wakiziandaa kwa njia ya udanganyifu pamoja na mihuri 159 na kuuzwa kwa bei ya shilingi elfu ishirini.
Watuhumiwa hao ni Athumani Selemani (71) ambaye anadaiwa kuwa amewahi kuwa mtumishi wa Serikali katika ofisi ya mkuu wa wilaya, Justine Mziray (55) anayetajwa kuwa ni mtaalamu wa kuchonga mihuri, Sporah Daud anayetajwa kushiriki katika uandaaji wa nyaraka hizo kwa kuchapa maandishi kwa kutumia mashine maalum pamoja na Costa Lyatuu anatajwa kuwa ni mtaalamu wa kughushi sahihi.
Nyaraka zilizokamatwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa, vyeti vya ubatizo, vyeti vya kliniki na matamko ya vizazi na vifo pamoja na mihuri mbalimbali ambayo imeonesha ni ile inayotumika wakati wa usajili vizazi na vifo katika manispaa ya Moshi na kitete mkoani Tabora.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, kamishna msaidizi wa polisi, Hamissa Issa amesema vifaa vingine vilivyokamatwa ni pamoja na mashine moja ya kuandikia na kifaa cha kuwekea namba.