Jumla ya watu 15, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma kwa tuhuma za mauaji ya Vijana wanne wa familia moja, ambao ni wafugaji katika kijiji cha Mbatamila Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo na migogoro ya wakulima na wafugaji nchini, Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP Simon Pasua hii leo September 24, 2022 amesema watu hao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi.
Amesema, Jeshi hilo limefanikiwa kukamata mifugo 159 iliyokuwa imeibiwa katika Kijiji cha Mbatamila Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma, na kwamba wanaendelea kushirikiana na wafugaji na wakulima kupambana na uhalifu.
Kwa upande wake katibu wa chama cha wafugaji nchini Bi. Prisca Kaponda, amesema wataendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya matumizi bora ya ardhi, ili kumaliza migogoro baina yao.
Baadhi ya wahanga wa tukio hilo, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwakamata watuhumiwa wa matukio ya mauaji na mifugo iliyokuwa imeibiwa na kuliomba Jeshi hilo kuongeza nguvu ili kupata mifugo ambayo haijapatikana.