Kamati ya Watalaamu wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais imekutana katika kikao cha siku moja kilichopokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mradi katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mtumba Jijini Dodoma kilihudhuriwa na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya zinatekeleza Mradi wa LDFS kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambapo pamoja na kupokea na kujadili taarifa hiyo, wajumbe wa kikao hicho pia walipitisha bajeti ya Mradi kwa mwaka 2023/2024.
Kikao kilichoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Waza Kiunsi pia kilipitia taarifa ya mradi na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wajumbe na namna bora ya utekelezaji wa bajeti ijayo ya mradi katika mwaka 2023/2024.
Mradi wa LDFS, miongoni mwa miradi kumi na mbili ya majaribio inayotekelezwa katika nchi kumi na mbili zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania. Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu zinatolewa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 7.156 na kusimamiwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo.
Katika Tanzania Mradi wa GEF unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai 2017 hadi Septemba 2022 katika Halmashauri za wilaya ya Kondoa Dodoma, Nzega (Tabora), Mkalama (Singida), Magu (Mwanza) na Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar.