Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini, wameitaka Jumuiya ya kimataifa kuangalia mwelekeo wa mkataba wa amani na ongezeko la ghasia miongoni mwa jamii.
Wataalamu hao, wametoa onyo hilo baada ya kuhitimisha ziara yao jijini New York, Marekani ambako wamepata fursa ya kuzungumza na maafisa mbalimbali.
Taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa, ya haki za binadamu iliyotolewa jijini Juba Sudan Kusini na Geneva, Uswisi imemnukuu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Sudan Kusini, Yasmini Sooka akisema wamezungumza na maafisa wa Umoja wa Mataifa ili kuwafikishia ujumbe huo.
Amesema, bila hatua hizo, kuna uwezekano wa kuona mamilioni ya wakimbizi wa ndani Sudan Kusini au wengine wakivuka mipaka na kusababisha ghasia kwa nchi Jirani na kwa mashirika ya misaada.
Hadi sasa, muundo wa mfumo wa uchaguzi haujabainishwa nchi humo, licha ya uchaguzi kuhitaji mazingira rafiki, na raia wa Sudan Kusini wanajaribu kuihoji serikali juu ya wanaofichua vitendo vya ukatili kupata vitisho vya kuuawa, kuswekwa korokoroni na kuteswa huku fursa za kisiasa zikizidi kubinywa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mkataba wa Amani ulijumuisha mchakato wa mashauriano ya kitaifa na kuanzishwa kwa Tume ya Ukweli, Maridhiano na Uponyaji ambayo yalifanyika katikati ya mwaka huu (2022), lakini yaliengua maeneo yaliyo chini ya upinzani pamoja na mamilioni ya watu waliokimbia kuhofia ya maisha yao.