Watu watatu wameripotiwa kuuawa baada ya jeshi kufyatua risasi za moto kuzima maandamano yanayofanywa na wafuasi wa chama cha upinzania cha MDC kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe.
Maandamano hayo yaliibuka baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza kuwa chama tawala cha Zanu-PF kimepata theluthi mbili ya wabunge wote. Viongozi wa upinzani walieleza kuwa Serikali imechakachua matokeo kwani wao wameshinda pia nafasi ya urais.
Hata hivyo, vurugu hizo zinaendelea wakati ambapo bado matokeo rasmi ya kura za urais hayajatangazwa. Nelson Chamisa wa MDC na Emmerson Mnangagwa wote wanadai wamepata kura za kutosha.
Umoja wa Mataifa na Uingereza ambayo iliitawala Zimbabwe, wamewataka wanasiasa kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo kuzua vurugu na kurejesha hali ya amani.
Waziri wa Uingereza, Harriett Baldwin ameandika kupitia Twitter, “tunafuatilia kwa karibu vurugu zinazoendelea #Harare. Tunatoa wito kwa viongozi wa kisiasa wa Zimbabwe kuwajibika na kuhakikisha utulivu katika wakati huu muhimu. Tunaangalia hali ilivyo kwa ukaribu,” #ZimbabweElections2018.
Naye Katibu Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Colm Cuanachain amesema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa kutumia jeshi baada ya uchaguzi ni kuingilia uhuru wa kujieleza na kukusanyika.
“Watu wanapaswa kupewa haki yao ya kufanya maandamano na kupinga,” alisema.
Hata hivyo, waziri wa mambo ya ndani wa Zimbabwe, Obert Mpofu ameonya kuhusu vurugu zinazoendelea na kueleza kuwa Serikali haitavumilia kuona amani inatoweka, hivyo watachukua hatua madhubuti.
“Wapinzani wanatujaribu, na nadhani wanafanya kosa kubwa. Hatutawavumilia,” alisema Mpofu.
Msemaji wa Chamisa amekosoa vikali matumizi ya jeshi kuzima maandamano pamoja na mauaji yaliyojitokeza.
“Wanajeshi wamefunzwa kuua wakati wa vita. Kwani wananchi wamekuwa adui wa nchi hii? Amehoji. “Hakuna sababu yoyote na kwa namna yoyote kufanya ukatili ulioonekana leo,” aliongeza.
Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wamekosoa ucheleweshwaji wa matokeo ya urais. Pia, katika ripoti yao wamesema wamebaini mapungufu kwenye uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na wapiga kura kutishiwa na Tume ya Uchaguzi kutoaminika.