Shirika la afya ulimwenguni (WHO), linafutiatilia taarifa za uwepo wa ugonjwa wa homa ya ini uliogundulika kwa baadhi ya watoto 700 wa nchi 34, ambao hadi sasa haijafahamika ni wa aina gani.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva nchini Uswisi, baada ya kupokea ripoti kuhusu mwelekeo wa ugonjwa wa Uviko-19.
“WHO imepokea ripoti za zaidi ya watoto 700 wanaoshukiwa kuwa na homa ya ini katika nchi 34 na wagonjwa wengine 112 wanachunguzwa,” amesema Dkt. Tedros.
Amesema, kwasasa takribani watoto 38 kati ya hao 700 wanahitaji kupandikizwa ini na kwamba watoto kumi kati ya hao wamefariki dunia.
Hata hivyo, WHO bado inaendelea kushirikiana na nchi zilizo na watoto hao waliobainika kuwa na ugonjwa wa ini, ili kuchunguza sababu halisi na kuweza kuwatafutia matibabu.
Dkt. Tedros anasema hadi sasa aina tano za virusi ambavyo hutambuliwa kusababisha homa ya ini havijagundulika miongoni mwa watoto hao, baada ya kuwafanyia vipimo.
“Kila mwaka, WHO hupokea taarifa za watoto kuwa na ugonjwa wa homa ya ini lakini baadhi ya nchi zimedokeza kuwa idadi ya watoto wanaogundulika ni kubwa kuliko ile iliyotarajiwa,” ameongeza Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia ugonjwa wa Uviko-19, Dkt. Tedros amesema idadi ya visa vipya na vifo imepungua, hali inayoleta matumaini kutokana na zoezi la utoaji chanjo linalosaidia kuokoa maisha.
“WHO na wadau tunaendelea kushirikiana na Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo kwa kuzipeleka watu walipo yaani mlango kwa mlango, gari kwa gari na kuhamasisha Viongozi wa kijamii,” amesisitiza Dkt. Tedros.
Kuhusu ugonjwa wa Monkeypox, Dkt. Tedros amesema zaidi ya watu 1,000 wamethibishwa kuugua ugonjwa huo katika nchi 29 na hakuna taarifa za kifo.
WHO, imeendelea kusisitiza na itatoa mwongozo kwa nchi utakaosaidia kuwezesha ufuatiliaji wa wagonjwa, kusimamia na uchunguzi huku wakitarajia kutoa mwelekeo wa tiba, udhibiti wa maambukizi na chanjo.