Imam mwenye ushawishi mkubwa jijini Khartoum nchini Sudan amezongwa na waumini akiwa msikitini wakimtaka awaongoze kufanya maandamano dhidi ya Serikali ya Rais Omar al-Bashir.
Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inawaonesha baadhi ya waumini wakipaza sauti mbele ya Imam huyo, “amka utuongoze kuandamana kutoka hapa msikitini.”
Umati wa watu walitoka msikitini wakipiga kelele za kutaka Serikali iliyopo madarakani iachie ngazi. Polisi waliofika katika eneo hilo walifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliojikusanya baada ya ibada ya Ijumaa.
Katika kipindi cha wiki mbili za maandamano ya kupinga Serikali, watu 22 wameripotiwa kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa Reuters, maandamano yaliyoshuhudiwa jana ni makubwa kuliko yaliyokuwa yamefanyika awali.
Maandamano yalianza Desemba 19 mwaka huu baada ya Serikali kutangaza kupanda kwa bei za vyakula na mafuta, hali inayodaiwa kuongeza gharama za maisha.
Nchi za Magharibi zimekuwa na kampeni ya kumkamata Rais al-Bashir ambaye ameiongoza Sudan tangu mwaka 1989. Anakabiliwa na mashtaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Nchi hiyo ilikuwa ikikabiliwa na vikwazo 20 vya Marekani pekee, hali inayozorotesha hali ya uchumi. Vikwazo hivyo viliwekwa kutokana na tuhuma kuwa inasaidia vikundi vya kigaidi.
Marekani iliondoa vikwazo hivyo mwaka 2017 lakini ilivirejesha tena baadaye kwa namna tofauti.