Polisi nchini Ethiopia kupitia Shirika la Utangazaji la nchi hiyo (EBC), imesema inamshikilia Mkuu wa shirika la kitaifa la kibinadamu la Ethiopia, Mitiku Kassakwa na washirika wake kwa tuhuma za ufisadi.
Mkuu huyo wa Tume ya Kitaifa ya Kudhibiti Hatari (NDRMC), wakala wa Serikali anayesimamia uzuiaji hatari na usaidizi wa waathiriwa, alikamatwa na polisi wa shirikisho hii Julai 13, 2022.
Katibu huyo wa Serikali wa usimamizi wa hatari, Mitiku alichukua wadhifa wa mkuu wa NDRMC mwaka 2015 na kuteuliwa tena Desemba 2019 kama mjumbe wa Jopo la Ngazi ya Juu la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu Uhamishaji wa Ndani.
“Anashukiwa kushirikiana na bosi wa Chama cha Elshadai kwa madhumuni ya ufisadi, Tadesse Ayalewe”, Naibu mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Kupambana na Ufisadi katika Tawi la Uhalifu la Polisi la Shirikisho, aliiambia EBC.
Kabla ya kukamatwa kwake, mshukiwa alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa polisi, ambao walikuwa wakichunguza nyendo zake na baada ya kukamilisha upelelezi ndipo walifanikisha kukamatwa kwake.
“Inajulikana kuwa chama hiki cha Elshadai kilipokea chakula na nguo mara kadhaa kwa manufaa ya watu waliohamishwa kutoka mikoa mbalimbali, lakini wenzake wakauza msaada huo ili kumnunulia mshukiwa nyumba,” amesema Afisa mmoja wa Polisi.
Ethiopia inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinadamu kutokana na athari za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ile iliyozuka katika eneo la kaskazini la Tigray Novemba 2020 na ukame usio na kifani katika mikoa kadhaa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu milioni 26, au chini ya robo tu ya wakazi wa nchi hiyo, wanahitaji msaada wa chakula ikiwa ni pamoja na karibu watu milioni tano waliokimbia makazi yao.