Wazazi wameaswa kuweka msukumo wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana walioko shuleni ili kuwajengea afya bora, kuepusha mimba za utotoni na zisizotarajiwa.
Wito huo umetolewa na Afisa wa mpango wa afya shuleni kutoka Wizara ya Afya, Magdalena Dinawi katika kikao kilichoandaliwa na wizara ya afya cha kujadili mpango wa kusogeza mahusiano na mawasiliano ya afya ya uzazi baina ya mzazi na mtoto mkoani Morogoro.
Amesema, ni jukumu la kila mzazi kutoa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana balehe kwani pamekuwepo na changamoto ya kutopata taarifa muhimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi kwa vijana .
“Ni jukumu letu kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana, kuna changamoto ya kukosa taarifa kuhusu mabadiliko na ongezeko la vichocheo mwilini hii inaweza kumpelekea kijana kujiingiza kwenye vitendo hatarishi vitakavyomsababishia madhara ikiwemo mimba za utotoni na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI.”
Awali, mkufunzi wa kitaifa wa afya ya uzazi kwa vijana Dkt. Taramael Ndossi amesema katika ulimwengu wa sasa kuna changamoto ya vijana kukosa malezi ya wazazi kutokana na muda mwingi kuutumia shuleni hivyo mpango wa elimu ya afya ya uzazi utasaidia kuelimisha wazazi na walimu namna nzuri ya kuwapatia elimu ya afya ya uzazi vijana walioko shuleni.
Alisema, “Mtoto anakaa bweni anakulia bweni ,kwa hiyo huu mpango wa elimu wa afya shuleni umekuja na wazo kuwa kumbe tunaweza tukaelimisha wazazi,tukaelimisha na walimu na kuwafundisha mbinu za mawasiliano ili waweze kuwasiliana na vijana wetu kuhusu afya ya uzazi.”
Kwa upande wao, wawakilishi akiwemo afisa maendeleo ya jamii mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, Victor Rugarabamu amesema jukumu la malezi kwa mtoto ni la mzazi, huku mwakilishi kutoka wizara ya Elimu Joel Mwamasangula akisema wazazi wasijisahau katika suala la malezi ya watoto shuleni.
Kikao hicho, kilichokutanisha wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, taasisi zilizo chini ya Wizara ya afya na wizara za kisekta ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum na Wizara ya Elimu.