Waziri mkuu wa utawala wa Taliban nchini Afghanistan Mohammed Hassan Akhund ameutetea utawala huo na kusema sio wa kulaumiwa kwa mzozo wa kiuchumi unaozidi kukithiri na kwamba unafanya kazi kukabiliana na ufisadi wa serikali iliyoondolewa.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa umma kupitia video ya nusu saa iliyopeperushwa na kituo cha habari cha serikali hii leo, Akhund pia amepuzia shinikizo la kimataifa la kuundwa kwa baraza la mawaziri shirikishi zaidi.
Akhund amesema kuwa matatizo ya ongezeko la ukosefu wa ajira na kudorora kwa uchumi yalianza chini ya serikali iliyopita iliyoungwa mkono na Marekani na kuongeza kuwa Waafghanistan hawapaswi kuamini madai kwamba utawala wa Taliban ni wa kulaumiwa.
Aidha kiongozi huyo amesema kuwa wameunda kamati kujaribu kutatua mzozo wa kiuchumi ulioko na kulipa malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi wa serikali ambao hawajalipwa kwa miezi kadhaa sasa.