Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua jengo la wagonjwa wa dharura kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa ambalo limegharimu Shilingi 390.72 milioni huku akisema ameridhishwa na ujenzi huo na uwepo wa vifaa vya kisasa.

Akizungumza na wakazi wa Ruangwa waliofika kushuhudia uzinduzi huo hii leo Machi 31, 2023 Waziri Mkuu amesema Hospitali hiyo imejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ambapo kazi ya ujengani wa uzio ni kubwa na kuwataka wakazi kuwa walinzi wa miundombinu na vifaa tiba vilivyonunuliwa ili waendelee kupata huduma bora na za uhakika.

Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel alisema Serikali ndani ya mwaka mmoja imetoa sh. bilioni 51.4 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za Taifa na Kanda ambapo kwa Mikoa ya nchi nzima, Rais alitoa shilingi 54.2 bilioni na kwenye eneo la vifaa shilingi 290.9 bilioni.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Afisa Muuguzi Shifra Buroko kuhusu
mashine ya usaidizi ya kupumulia baada ya kuzindua Jengo la Wagonjwa wa Dharura la
Hospitali ya wilaya ya Ruangwa hii leo Machi 31, 2023.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi – OR-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema jengo hilo lililozinduliwa ni miongoni mwa majengo 80 yaliyojengwa nchini kwa kutumia fedha za UVIKO-19. Katika mkoa wa Lindi, majengo kama hayo yamejengwa pia katika wilaya za Liwale na Kilwa.

Alisema, katika awamu ya kwanza, wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni 2.9 ambazo majengo yake yamekamilika na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta sh. milioni 800 za kujenga wodi za kisasa ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa pia.

Naye, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dkt. Salvio Wikesi alisema mradi huo unatarajiwa kuwa na majengo 22 ambayo hadi kukamilika kwake yanatarajiwa kugharimu sh. bilioni 7.5 na kwamba kiasi cha shilingi 90.72 milioni zilitumika kuimarisha eneo la Hospitali lililokuwa na maji mengi chini ya ardhi.

Ndalichako akagua maandalizi uzinduzi mbio za Mwenge 2023
Polisi Tanzania FC: Tunabaki Ligi Kuu