Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini Geita yameendelea kuwanufaisha wakazi wa Geita na viunga vyake baada ya wananchi na wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali kujitokeza kupata elimu pamoja na kufanyiwa uchunguzi saratani.

Huduma hiyo inayoendelea kutolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita kwa ushirikiano na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), inahusisha upimaji wa satarani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume huku hatua hiyo ikija wakati dunia ikielekea katika mwezi Oktoba ambao ni wa uelimishaji kuhusu saratani ya matiti.

Wakizungumza na mwandishi wetu katika banda linalotoa huduma hizo kwenye Viwanja vya Bombambili -EPZ Mjini Geita, mmoja wa wananchi hao, Neema Mgase ambaye ni mkazi wa Nyamalembo mkoani Geita mbali na kuelezea huduma nzuri alizozipata alishauri wakazi wa mkoa huo wafike kupata huduma hizo hasa ikizingatiwa ni bure.

“Wanawake tunapitia changamoto mbalimbali ikiwamo uzazi na nyingine ndio maana nikaona nije kupata uchunguzi, wito kwa kampuni nyingine ni kusaidia jamii ya watanzania ambao wengi tupo katika hali duni kutokana na umaskini kuwekeza kwenye huduma kama hizi ili kusaidia kuboresha afya kwa jamii,” alisema.

Naye Mzee Masele Athumani ambaye ni mkazi wa Nyantorotoro A, alisema amehamasika kufanya uchunguzi wa saratani ya tezi dume hasa ikizingatiwa yupo kwenye umri ambao anaweza kunyemelewa na magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani huku akiwataka wakazi wa Geita kujitokeze kwa wingi kujua afya.

Kwa upande wao wafanyakazi wanawake wa kampuni ya  GGML nao walifanyiwa uchunguzi wa saratani akiwamo, Muuguzi katika hospitali ya GGML, Chitegetse Rushatsi ambaye alisema ameamua kwenda kupata elimu na kufanya uchunguzi wa saratani kwa sababu anatamani kutembea akiwa anajiamini.

“Saratani haioneshi dalili, kitakachokufanya ujue hauna saratani ni kupima tu, na sio njia nyingine yoyote ndio maana nimeshawishika kwenda kupima nijiamini, wito wangu kwa wanawake wapime kwa sababu huwezi jua una saratani kwa kutembea isipokuwa pale utakapoanza kuonesha dalili na ukishaanza kuonesha dalili hapo saratani imefikia hatua ambazo ni ngumu kutibiwa,” alisema.

Naye Happy Ijumba ambaye pia ni mfanyakazi wa GGML alisema “kwa sababu saratani si ugonjwa wa kawaida, na kwa sisi wanawake mpaka upate dalili kuona viashiria ujue tayari umeshakuathiri, ndio maana nikaona umuhimu kuja kupata vipimo kujua kama nimepata hivyo virusi au la.”

Akizungumzia utoaji wa huduma hizo, Mratibu wa huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita, Dk. Pasclates Ijumba alisema wameamua kutoa huduma hizo ili kudhibiti madhara ya saratani hususani kwa wananchi ambao wamekuwa waoga kufanyiwa uchunguzi kutokana na na dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii.

Alitoa mfano kuhusu chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo hutolewa kwa mabinti wadogo, baadhi ya jamii huwazuia watoto wao kupatiwa chanjo hiyo kutokana na ukosefu sahihi wa elimu kuhusu chanjo hiyo.

Simba, Young Africans zimeleta AFCON 2027
Serikali yataka kasi usambazaji wa Umeme Vijijini