Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema suala uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa nchi na kutaka kila Mtanzania azingatie uhifadhi wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 16, 2023 wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya maji na mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Usambazaji Maji kati ya Makongo na Mji wa Bagamoyo uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Tegeta A, jijini Dar es Salaam.
Amesema, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu ya ukusanyaji na usambazaji wa maji, ni jukumu la kila Mtanzania kutunza vyanzo vya maji. “Tuna jukumu kubwa nalo ni la kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji; na eneo hili tuna mgogoro mkubwa kwani vyanzo vyetu vya maji vinaharibiwa, ni wajibu wetu kutunza vyanzo hivi.”
“Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameshatoa mwongozo wa uhifadhi wa vyanzo vya maji na kila Mtanzania anapaswa kuzingatia hilo tunahitaji kuweka nguvu moja katika kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za maji. Nitoe wito kwa Wizara, wadau wa maji na wananchi tutunze vyanzo hivi iwe ni visima, mito, au mifereji vyote tuvilinde,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa, “suala la uhifadhi ni muhimu sana. DAWASA isimamie suala hili kwa karibu na kutoa taarifa mapema. Wakurugenzi wa Mabonde ya Maji nchini kama vile Ruvuma, Rufiji, Malagarasi na mabonde mengine yote hakikisheni mnafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili vyanzo hivi visiharibiwe. Wananchi tulinde vyanzo hivi na mtu akionekana anaharibu, kama ni kisima au chanzo kingine, tuchukue hatua, tusisite kwa sababu huo ni uhujumu.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Maji Jumaa Aweso alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Kiula Kingu ahakikishe wananchi wote walioomba maji wafungiwe mita ndani ya siku saba kama Mkataba wa Huduma ya Wateja unavyosema.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wizara yake, Waziri Aweso alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye wizara hiyo ambazo ni mahsusi kwa utekelezaji wa miradi ya maji. “Mheshimiwa Rais kwa sasa ametoa asilimia 90 ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maji, wakati awali utekelezaji ulikuwa ni kati ya asilimia 50 hadi 60,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bibi Preeti Arora alisema mradi huo ulilenga kuongeza upatikanaji wa maji na kwamba ameridhishwa kuona fedha zilizotolewa zinasimamiwa kwa karibu na Serikali ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji yameanza hii leo Machi 16 na yatahitimishwa Machi 22, 2023 yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Kuongeza Kasi ya Mabadiliko katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo endelevu ya Uchumi.”