Waziri wa Nchi (OWM-Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania – ATE wataendelea kusimamia sheria za kazi na masuala ya ajira nchini na kuweka mazingira rafiki katika sehemu za kazi.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo wakati alipokuwa akimkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwanamke Kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Amesema, “kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania – ATE tutaendelea kusimamia sheria za kazi na masuala ya ajira nchini na kuweka mazingira rafiki katika sehemu za kazi na hii itasaidia kuleta mabadiliko katika teknolojia.”
Kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara kwenye sekta binafsi, Prof. Ndalichako amesema, “utekelezaji wa Kima cha Chini ulianza tarehe 1 Januari, 2023. Niwasihi ATE iendelee kutoa elimu na kuwasimamia wale ambao bado hawajatekeleza kikamilifu kwani hiyo ni haki ya kila mfanyakazi.”