Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa vibali kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili waweze kwenda kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yote ya kutolea huduma hizo zikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Majaliwa ameyasema hayo leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyetaka kufahamu ni upi mpango wa Serikali katika kuhakikisha miundombinu iliyopo katika maeneo ya kutolea huduma za afya na vifaa vinaendana na utoaji huduma wa uhakika kwa kupitia uwepo wa wataalamu wa kutosha.
Amesema, hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za Halmashauri za Wilaya, mikoa na kanda na kuongeza kuwa, “tutaendelea kuimarisha maeneo hayo ya utoaji huduma na Serikali itaendelea kujenga miundombinu kulingana na mahitaji ya eneo husika.”
Aidha, Majaliwa amesema mpango mwingine wa Serikali katika kukabiliana na changamoto ua upungufu wa watumishi kuwa ni pamoja na kufanya mapitio ya ikama ya watumishi na kwa kuhamisha watumishi katika maeneo yenye watumishi wengi na kuwapeleka kwenye upungufu.