Mabingwa wa soka Tanzania bara, Young Africans wanajitupa kwenye Uwanja wa Sagrada Esperanca mjini Dundo, Angola jioni ya leo kumenyana wenyeji, Sagrada Esperanca katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza Saa 9:00 Alasiri kwa saa za Angola na Saa 11:00 jioni kwa Saa za Tanzania.

Young Africans iliwasili Dundo usiku wa juzi baada ya safari ya kutwa nzima wakipitia Luanda, ambako waliunganisha ndege nyingine kwa saa mbili kuja mjini wa wenyeji wao, Sagrada Esperanca.

Young Africans iliyofikia katika hoteli ya bora zaidi mjini humo, Diamante, itahitaji sare ili kuingia hatua ya makundi, baada ya awali kushinda 2-0, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony wiki iliyopita Dar es Salaam.

Kocha Mholanzi wa Young Africans, Hans van der Pluijm amesema kwamba ana imani kurejea kwa wachezaji wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma kutaiogezea nguvu timu yake.

Wawili hao waliukosa mchezo wa kwanza kutokana na kuwa wanatumikia adhabu ya kadi za njano walizopewa kwenye mechi mfululizo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwezi uliopita Dar es Salaan na Cairo, Young Africans ikitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini.

Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.

Young Africans imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.

Young Africans ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.

Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.

Vikosi vya leo vinatarajiwa kuwa; Young Africans; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.

Sagrada Esperanca; Yuri Jose Tavazes, Roadro Juan da Semero, Dennis Conha Morais, Asenio Cabungula, Antonio da Silva Oliveira, Ntaku Zabakaka, Manuel Paulo Joao, Alentua Tangala Rolli, Osvaldochitumba Palana, Manuel Sallo Conha na Antonio Kasule.

Ndoa Ya Azam FC Na Stewart John Hall Yavunjika Rasmi
Beef: Vanessa, Shilole watupiana matusi ‘makavu’