Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar limeahidi kuwasindikiza kwenye vituo vya kupigia kura watu wote wanaotaka kupiga kura lakini wanahofia usalama wao kutokana na vitisho vilivyopo, katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika kesho (Machi 20).

Hali ya usalama visiwani humo bado inatia kizunguzungu kutokana na kuwepo kwa ripoti tofauti tofauti za matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na kulipuliwa kwa mabomu. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam amekiri kuwepo kwa vitisho hivyo na kuahidi kuvikabili.

“Kuna vitisho. Lakini kama mtu yoyote anataka kupiga kura lakini anahisi maisha yake yatakuwa hatarini, anaweza kutupa taarifa na tutamsindikiza kwenye kituo cha kupigia kura na akimaliza tutamsindikiza kurudi nyumbani, alisema Kamanda Mkadam na kuongeza kuwa wametoa namba zao za simu kwa umma.

Aliongeza kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika maeneo yote hadi ndani ya vituo vya kupigia kura na umbali wa mita 200 kutoka kwenye vituo hivyo.

Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi waandamizi wa Chama Cha Wananchi (CUF), Kamanda Mkadam alisema bado wanawashikilia kwakuwa wanataka kupata taarifa muhimu za kiusalama kutoka kwao ikiwemo ile ya ulipuaji wa mabomu katika nyumba ya Kamishina wa Jeshi hilo na katika Maskani ya CCM, Unguja.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui alisema kuwa kitendo cha kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho ni muendelezo wa ubabe na ukandamizaji dhidi ya chama hicho kutokana na msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio kwani uchaguzi halali ulishafanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Zanzibar: Mwandishi wa DW apotea uwanja wa Ndege
Yaya Toure Kuwavaa Suadan Juma Lijalo