Joto la uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar linazidi kupanda ikiwa imebaki siku moja, ambapo jana Mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Ujerumani (DW), Salma Said alikamatwa katika uwanja wa ndege na watu wasiojulikana (ingawa wanadaiwa kuwa wanausalama) na hadi sasa hajulikani alipo.

Taarifa iliyotolewa na na mume wa mwandishi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ali alisema kuwa alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa mkewe jana kuwa amekatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Unguja, alipokuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kupata matibabu.

Alisema kuwa mkewe alikamatwa majira ya saa 8:05 mchana, dakika chache baada ya kucheleweshwa kwa ndege aina ya Auric.

“Ndege ilicheleweshwa karibu nusu saa, abiria wakaelezwa ndege inasubiri kwanza. Ndipo walipokuja polisi na kumchukua,” Ali anakaririwa.

Hata hivyo, ingawa Ali anadai kuwa mkewe alichukuliwa na Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam amedai kuwa hana taarifa yoyote kuhusu kukamatwa kwa mwandishi huyo na jeshi lake.

Siku chache zilizopita, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Zanzibar, Salum Msangi alisema kuwa Jeshi la Polisi lina orodha ya majina ya watu wanaotakiwa kuhojiwa wakiwemo waandishi wa habari.

Chidi Benz aweka wazi kinachomkondesha, aomba msaada
Zanzibar: Polisi Mkono kwa Mkono na wapiga kura