Meneja wa klabu bingwa barani Ulaya, Real Madrid Zinedine Zidane amepasua ukweli kuhusu mikakati yake ya kutaka kumsajili kiungo kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Juventus na Italia, Paul Pogba.

Pogba amekua gumzo katika kipindi hiki, na tayari klabu ya Man Utd ambayo inanolewa na meneja kutoka nchini Ureno Jose Mourinho inaongoza kwenye harakati za usajili wa kiungo huyo.

Real Madrid walikua wakitajwa katika mbio hizo, lakini kulikua hakuna uhakika wa asilimia 100 kutokana na kauli za viongozi wa klabu hiyo ya mjini Madrid nchini Hispania, kutosikika kupitia vyombo vya habari hukusu mpango wa usajili wa Pogba.

Kauli ya Zidane aliyoitoa katika mkutano na waandishi wa habari akiwa mjini Montreal nchini Canada, ambapo kikosi cha Real Madid kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi, imedhihirisha ukweli wa jambo hilo ambalo sasa linaibua ushindani dhidi ya Man Utd.

Zidane alijikuta akiweka wazi mpango huo, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kama ana anatamani kuwa na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 kikosini kwake, ambapo alijibu ni kweli anahitaji kuwa na mchezaji kama huyo.

“Ninatamani kuwa na Pogba na ningependa kumuona akicheza katika kikosi changu, ni mchezaji mzuri na kila klabu inamuhitaji kutokana na ubora wake uwanjani.” Alisema Zidane

Kikosi cha Real Madrid kimeweka kambi nchini Canada, na kinatarajiwa kucheza michezo ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, Chelsea pamoja na FC Bayern Munich.

Timu hizo zitacheza michezo hiyo ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kupitia michuano ya Champions Cup.

Klabu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo kwa mwaka huu ni FC Barcelona, Celtic, Liverpool, Inter Milan, AC Milan pamoja na Leicester City.

Wakazi awaweka mkao wa kula mashabiki kuipokea Album yake
Alikiba na Diamond Wajifunze Kupitia Maneno ya Jokate Mwegelo