Mkurugenzi wa kuratibu na kukuza utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, (NIMR) Dkt. Paul Kazyoba, amesema kuwa kabla ya kupata chanjo, ni muhimu mtu asitumie kilevi kabla na baada ya kuchoma chanjo kwa saa 72
Amesema hayo wakati akizungumza na kituo cha habari cha EATV, ambapo amesema kuwa siku moja kabla ya kupata chanjo usitumie vilevi, ili kuufanya mwili wako uwe huru.
“Kuufanya mwili uzalishe hizi seli kinga, inatakiwa usiingiliwe na kitu chochote cha tofauti kwenye damu kwa saa 72. Kilevi cha aina yoyote kwa maana ya pombe, bangi, shisha au dawa za kulevya lazima kitaingilia mfumo na hivyo kuifanya chanjo kutofanya kazi yake vizuri”, amesema Dkt. Kazyoba.
“Ndani ya saa 72 ni muda ambao kazi kubwa inafanyika, ndiyo maana maudhi madogo madogo mtu anayapata ndani ya muda huo, vilevi vitaathiri uzalishaji wa mwanzo wa seli za kinga, ambazo zitajitengeneza mwilini mwako kwa miezi kadhaa,” amesema Dkt. Kazyoba.
Baada ya mtu kupata chanjo miongoni mwa mambo ya kuzingatia yanayosisitizwa ni kutopata kilevi cha aina yoyote kwa muda wa saa 72 sawa na siku tatu.