Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limemzuia Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwanga Community Center ambao ulipaswa kufanyika leo Januari 16, 2018.
Katika taarifa iliyotolewa na OCD imesema kuwa kiongozi huyo hakufuata utaratibu wa kutoa taarifa ndani ya masaa 48 kabla ya kufanyika kwa mkutano huo jambo ambalo Zitto amelilalamikia na kusema kuwa amezuiwa kufanya mkutano huo kinyume na sheria ya Bunge ya mwaka 1988,
“Mimi sitaki kuwapa Polisi sifa ya kupambana nasi. tumeahirisha mkutano mpaka siku ya jumamosi Lakini tumewaandikia barua rasmi kuwa sheria waliyonukuu sio sheria halali na haihusiani na mikutano ya Mbunge kwenye jimbo lake la Uchaguzi. Sheria wanayopaswa kunukuu ni sheria namba 3 ya mwaka 1988 kifungu cha 4(1),”amesema Zitto,
Hata hivyo, Zitto Kabwe amedai kuwa atamwandikia barua rasmi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuhusu suala hilo ili kutengeneza mazingira kwa siku za usoni lisije kumtokea Mbunge mwingine yoyote.