Mwanamuziki nyota wa WCB, Zuhura Othman Soud anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii ‘Zuchu’ bado anabakia kinara kwa kuweka historia ya kuwa msanii mwenye wimbo uliotazamwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube kwa mwaka 2021.

Wimbo uitwao ‘Sukari’ alioutoa Januari 30, 2021 hadi sasa umefikisha watazamaji zaidi ya milioni 61, na kuwa wimbo pekee uliotazamwa zaidi katika ukanda wa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mwaka 2021.⁣

“SUKARI, Wapenzi Milioni 60,000,000? Watazamaji Milioni 60,000,000 kwenye youtube. Wimbo wa Kiafrika uliotazamwa zaidi kwenye YouTube mwaka wa 2021 Am grateful And humbled.Asanteni nawapenda ?? Asante @iam_trone,” aliandika Zuchu.⁣

Aliongeza kuwa; “Ikumbukwe Tangia Tanzania Itapate Uhuru, Zuchu ndio msanii Peke mwenye wimbo wenye watazamaji wengi akiwa peke yake bila ushirikiano akifuatiwa na Jeje ya Diamond Platnumz,”.

Mnamo Machi 2021, mwimbaji huyo alifanikiwa kuingia kwenye rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kupata idadi ya wafuatiliaji ‘Subscribers’ milioni 1 kwenye mtandao wa YouTube, na pia alikua msanii wa kwanza wa kike barani Afrika kufikia hatua kama hiyo ndani ya miezi 11 tangu kutambulishwa rasmi kwenye tasnia ya muziki.

Juni 17, 2021, Zuchu alikuwa msanii wa kwanza wa kike kwa ukanda wa Afrika Mashariki kutunukiwa Golden Plaque na mtandao wa YouTube baada ya channel yake kufika na kuvuka idadi ya watu milioni 1 wanaofuatilia channel hiyo.⁣

Zuchu ambaye alitambulishwa rasmi kama msaini wa WCB mnamo Aprili 2020, amekuwa akijiwekea na kuvunja rekodi zake kwa miezi michache tu kwenye tasnia ya muziki.

Yeye ni msanii wa pili wa kike chini ya WCB baada ya Queen Darleen ambaye alisainiwa mwaka 2016.

Mnamo Juni 2020, Zuchu alilitumbukiza jina lake katika vitabu vya historia nchini Tanzania na Afrika Mashariki, kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike kutunukiwa tuzo ya Silver Plaque miezi miwili tu baada ya kujiunga na mtandao wa youtube.

Oktoba 2020, Zuchu alikuwa miongoni mwa wasanii watatu kutoka Tanzania ambao ni Diamond Platnumz na Rayvanny walioingia kwenye orodha ya wasanii wa kuzingatiwa kwenye Tuzo za Grammy 2020 ‘Grammy Awards Consideration’.

Bado zimesalia takribani siku nne kuumaliza mwaka 2021 Je kuna lolote litabadilika kwenye rekodi hizi alizoziweka Zuchu kwa mwaka huu ???

P Square wawaomba radhi mashabiki
Waziri wa Afya Zanzibar apata dalili za Corona