Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Tanzania Aishi Manula ametajwa kwenye kikosi cha wachezaji 11, waliofanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zinazoendelea nchini Cameroon.

Manula ametajwa kwenye orodha hiyo, baada ya kuonesha uwezo mkubwa wa kulinda lango la Taifa Stars kwenye michezo mitatu ya hatua ya makundi, ambapo Tanzania walicheza dhidi ya Zambia, kisha Namibia na kumaliza dhidi ya Guinea.

Mlinda mlango huyo wa klabu ya Simba SC amekua mtanzania pekee kwenye orodha ya wachezaji waliotajwa kwenye kikosi hicho ambapo upande wa mabeki ni Issiaka Samake (Guinea), Henoc Inonga Baka (DR Congo), Adrian Chama (Zambia) na Hamza El Moussaoui (Morocco).

Viungo ni Amede Obenza Masasi (DR Congo), Salomon Charles Banga (Cameroon), Chandrel Massanga (Congo Brazzaville)  na Victor Kantabadouno (Guinea).

Washambuliaji ni Soufiane Rahimi (Morocco) na Gnagna Yakhouba Barry (Guinea).

Fainali za ‘CHAN’ zinaingia hatua ya Robo Fainali baada ya michezo ya hatua ya makundi kukamilishwa jana Jumatano (Januari 27) kwa michezo ya kundi D.

Hatua ya Robo Fainali itaanza rasmi keshokutwa Jumamosi (Januari 30), ambapo Mali watacheza dhidi ya Congo Brazzaville huku wenyeji Cameroon watapambana dhidi ya mabingwa mara mbili wa michuano hiyo DR Congo.

Jumapili (Januari 31) Guinea watapapatuana dhidi ya Rwanda na Morocco watapambana dhidi ya Zambia.

PSG wamng'ang'ania Dele Alli
Rais Magufuli amsamehe Mkurugenzi aliyenunua gari la kifahari