Tanzania itacheza na Ivory Coast kuwania kufuzu kwenye fainali za Soka ya Ufukweni nchini Nigeria baadaye mwaka huu.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa imesema kwamba mchezo wa kwanza utafanyika Abidjan kati ya Agosti 26, 27 na 28.8.2016 na marudiano yatafanyika Dar es Salaam kati ya Septemba 16, 17 na 18, mwaka huu.

Timu nyingine zilizomo kwenye kinyang’anyiro hicho mbali ya Tanzania na Ivory Coast ni Cape Verde, Ghana, Misri, Liberia, Libya, Kenya, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Senegal, Sudan na Uganda.

Kutakuwa na mechi moja moja tu za kuwania kufuzu ambapo washindi saba wataungana na wenyeji Nigeria kwenye fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Desemba 13 hadi 18, mwaka huu.

Timu zitakazoingia fainali ya michuano hiyo, zitaiwakilsha Afrika kwenye Kombe la Dunia la FIFA la Soka ya Ufukweni ambalo fainali zake zitafanyika Bahamas kuanzia Aprili 27 hadi Mei 7 mwaka 2017.

Madagascar ndiyo walikuwa mabingwa wa mwaka 2015 baada ya kuifunga Senegal kwa penalti 2-1 kwenye fainali nchini Shelisheli.

Serikali Kulinda Afya Ya Jamii
Wizara Ya Ardhi Yavunja Rekodi Ukusanyaji Mapato