Diamond Platinumz leo aliamua kutoa ya moyoni kuhusu jitihada alizozifanya za kukata mzizi wa fitina kibiashara kati yake na upande wa mshindani wake, ‘Mfalme’ Ali Kiba.

Mmiliki huyo wa lebel ya WCB ameweka wazi kuwa amekuwa akitafuta jinsi ya kufanikisha shindano kubwa uwanja wa Taifa kumsaka mkali kati yake na upande wa mshindani wake huyo, lakini wamekuwa wakikwepa.

“Hao watu wanaosema ni wakali, nilishawaomba collabo tufanye wamenikimbia. Nimeshaomba show na menejimenti yao tufanye show ‘Mkali Nani’… hii Desemba nilitaka niifanye uwanja wa taifa mimi na wao, tuone nani mkali, wamekataa,” alifunguka.

“Juzi nilikuwa na January Makamba, nikamwambia ‘Makamba hebu tudhaminie hii show tufanye mkali nani Tanzania nzima’, hawataki wanakimbia… sasa wewe mkali unakimbia! Njoo..,” alisema.

Ingawa mtangazaji wa XXL, B12 aliamua kuweka wazi kuwa msanii huyo ameamua kusema na mahasimu wake kimuziki, Ali kiba na Ommy Dimpoz, na kwa hili haswa mlengwa ni Mfalme Kiba, hakutaka kumung’unya maneno kupinga.

Alisisitiza kuwa ingawa wanasema yeye anafanya muziki kiujanjaujanja na kwamba anazidiwa sauti, yeye hutumia akili zaidi yao na kwamba muziki wa sauti bila kutumia akili ni kupiga makelele.

“Kama muziki ni sauti, basi ningemsaini Wema Sepetu,” alisema.

Miezi michache iliyopita, rapa King Crazy GK alisema kuwa angepewa kusimamia bifu kati ya Ali Kiba na Diamond wangeingiza pesa nyingi na kwamba angehakikisha wanafanya show moja kubwa katika uwanja wa Taifa kumsaka ‘mkali zaidi’, wazo ambalo kumbe limekuwa likifanyiwa kazi na Diamond.

Katika hatua nyingine, Diamond ametangaza habari njema na kubwa kwa mashabiki wake kuwa yeye na lebel yake kwa pamoja wamesaini kuwa chini ya lebel kubwa duniani ya Universal Music Group (UMG).

Amesema kuwa lebel hiyo inayosimamia kazi za lebel nyingine kubwa kama Aftermath Records ya Dr. Dre, Def Jam Records na nyingine, imetoa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1 (zaidi ya shilingi bilioni 2 za Tanzania) kwa ajili ya kusambaza kazi zao duniani.

Diamond ameeleza pia hatua nyingine kubwa aliyoipiga kuwa ataachia albam yake mwezi ujao ambayo ndani yake kuna kazi alizofanya na Rick Ross pamoja na Rihanna! Ndiyo… Robyn Fenty aka Rihanna.

Ligi Ya Mabingwa Barani Ulaya
Video: Rais Magufuli anafanya kazi nzuri sana - Mwinyi