Uongozi wa chama cha soka Dodoma (DOREFA), umeahidi kufanya kazi bega kwa bega na viongozi wa Dodoma FC ili kufanikisha mpango wa kuwa na kikosi bora, ambacho kitakuwa na uwezo wa kupambana vilivyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa DOREFA  Mulamu Ngh’ambi, amesema watahakikisha wanashirikiana na viongozi wa klabu hiyo ili kufanikisha usajili wachezaji wachache wapya kwa kuzingatia maeneo ambayo wamebaini yana  upungufu kwa kuongeza wachezaji wenye uzoefu.

Ngh’ambi amesema moja ya makosa ambayo timu nyingi zinazopanda daraja na kucheza Ligi Kuu ni kukibadilisha kikosi karibuni chote kilichopanda na kusajili wachezaji wengi ambao wanaowaona ni wazoefu, lakini kutimua makocha waliozipandisha timu hizo.

“Katika kujenga timu ni lazima uwe na vitu viwili au vitatu. Uwe na timu ya msingi ambayo umepanda nayo, halafu baadaye ndiyo kuangalia aina gani ya wachezaji ambao wanaweza kuboresha timu iliyopo ili iweze kushindana, lakini kwa sasa haipo hivyo, mpira umebadilika sana,” amesema kiongozi huyo.

Mwenyekiti huyo mesema Makata ni kocha anayeamini kuwajenga wachezaji vijana ambao ametoka nao chini na hajatofautiana na Juma Mgunda wa Coastal Union ambaye idadi kubwa ya wachezaji alionao ni wale walioipandisha timu hiyo.

“Changamoto imekuwa ni tabia ya viongozi kutowaamini walimu ambao wanapandisha timu, wao anaona viwango vyao ni vya kupandisha tu na baada ya hapo wanawaacha,” alisema.

Mwishoni mwa juma lililopita, Dodoma FC ilitwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara baada ya kuifunga Gwambina FC bao 1-0 katika mchezo wa fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini, Dar es Salaam.

Aston Villa yafufua matumaini EPL
Diamond akabidhi kompyuta kwa watoto yatima