Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege, Iringa itakuwa inapokea ndege kubwa zinazoweza kubeba abiria kuanzia 70.

Rais Samia amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Iringa Leo Agosti 12, 2022.

Picha na Ikulu Mawasiliano

Rais Samia amesema adhma ya Serikali ni kufanya marekebisho na kuendeleza aina zote za usafiri ili kukuza biashara na kutoa fursa pana ya usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa na hatimaye kukuza biashara ndani na nje ya nchi.

“Iringa ni wazalishaji wazuri wa chai, mazao ya mbao na parachichi, hivyo uwanja huu ukikamilika mazao haya yatakuwa na fursa nzuri ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi na ndani ya nchi ambapo mazao haya yanahitajika,” amesema Rais Samia.

Aidha ameongeza kuwa, “Uwanja huu utaleta utalii wa kutosha Iringa kwani tuna vivutio vingi ambavyo bado havijafunguliwa kwa utalii.”

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mhandisi Rogatus Mativila, amesema kutokana na umuhimu wa kiwanja cha ndege cha Iringa kwa shughuli za biashara na utalii, Serikali imekuwa ikikifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili kiweze kuhudumia abiria kwa usalama.

“Kiwanja hiki ni miongoni mwa viwanja 11 vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 1.13.”

Amesema Mkataba wa mkopo kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia umeshasainiwa na kwa sasa TANROADS inajiandaa kwa ajili ya kutangaza zabuni.

Kiwanja hicho kinajengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 63,7 na Mhandishi Mshauri kutoka TANROADS atasimamia mradi kwa gharama ya Shilingi milioni 848.1.

Mradi unatarajiwa kukamilika Agosti 26, 2023.

Mgogoro wafukuta ujenzi mradi tata wa umeme
Kenya: Waangalizi wa uchaguzi wadai kutengwa