Rais wa John Pombe Magufuli amemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Dawa hizo nchini.

Majaliwa amekabidhiwa kazi hiyo leo Februari 12, 2017 wakati wa kuapishwa kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter Makakala, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers William Sianga pamoja na mabalozi watatu, Omary Yusuph Mzee, Joseph Edward Sokoine pamoja na Grace Aron Mgovano aliowateua hivi karibuni Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Elimu ana Mafunzo ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

“Nalipongeza sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika mstaafu, Mhe. Anne Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya kuona sheria za mwanzo za kupambana na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo Wabunge wa wakati ule walisimama kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt. Magufuli.

Pia, Rais Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kusaini sheria hiyo haraka mara baada ya Bunge hilo kuipitisha kwa sababu alijua madhara ya dawa za kulevya katika nchi yetu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa limeendelea kushuhudia kizazi chetu kikiendelea kudidimia kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya na Serikali kwa mipango yake imeendelea kukemea, kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizo.

“Jambo hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana wetu wengi wamepoteza uwezo wa kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa sababu baada ya matumizi tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa mwili, uwezo wa kutafakari pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi kikubwa linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya nchi hivyo jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo yetu kwa ujumla wake.

Alisisitiza zaidi kuwa vita hii ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa hadi imalizike hivyo Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja anatakiwa kushiriki kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi hii.

Yanga yaipeperusha vyema bendera ya tanzania ugenini
Video: Gwajima kumshtaki Makonda kwa Rais Magufuli