Geita Gold Mining Limited (GGM), kwa mwaka wa tano mfululizo imejitosa kuwa mdhamini mkuu wa Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini ambayo mwaka huu yanafanyika katika viwanja vya Ukanda wa Uwekezaji (EPZ) Bombambili mkoani Geita.

GGML imekuwa mdhamini mkuu, katika maonesho hayo yanayotumika kuonesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji pamoja na kuwezesha kliniki za biashara kwa wajasiriamali na kampuni zenye uhitaji na fursa zinazopatikana katika mgodi wa GGML.

Maonesho hayo yaliyoanza Septemba 27, 2022 yatafikia tamati Oktoba 8, 2022, ambapo yatatoa fursa kwa washiriki kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa katika uchimbaji wa madini huku GGM ikiungana na kampuni 600 zinazoshiriki kwa mwaka huu ikiwa na mifumo na teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuwaonesha wadau hususani wachimbaji wadogo.

Akizungumzia udhamini wa GGML katika maonesho hayo, Makamu Rais wa Kampuni Anglo Gold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa nchi za Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema kampuni hiyo inafarijika kuwa mdhamini mkuu wa maonesho hayo yaliyoanza miaka mitano iliyopita.

Amesema, “Tunafarijika kwamba tulihusishwa kama mmoja wa wadhamini wakubwa kuanzia mwanzoni lakini pia tunatambua kwamba wadau wengine ambao hawapo hata kwenye sekta ya madini kama mabenki na wadau wengine waliona umuhimu wa kushiriki si tu kudhamini lakini pia kuleta bidhaa zao kwenye maonesho haya na kuzionesha.”

Mapema mwaka huu, kampuni ya GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini kwa mwaka wa fedha 2020/2021, baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira, usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 30, 2022
Waandamana kutaka uhalali watoe mimba