Tanzania, imesema inatekeleza mfumo wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali, ambao utahakikisha sekta zote za uchumi zinatumia TEHAMA, huku ikiwezesha mabadiliko hayo yanayojenga jamii jumuishi kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akiwasilisha tamko la Kisera la Tanzania, katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano Duniani (ITU PP 2022), unaofanyika Bucharest, Romania.

Amesema, Tanzania ina Sera ya Taifa ya TEHAMA, ambayo imesababisha ongezeko kubwa la matumizi katika sekta mbalimbali za uchumi na kuwe imewezesha ujumuishaji wa kifedha unaohusisha idadi ya Watanzania ambao hawakuwa wanapata huduma za kibenki hasa jamii ya vijijini.

Nape ameongeza kuwa, “Tangu tuanzishe Mfumo wa Leseni uliounganishwa mwaka 2005 ili kuinua TEHAMA katika jitihada zetu za kuinua ustawi wa kijamii na kiuchumi wa watu wetu, tumeona mafanikio, shukrani kwa mikakati ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.”

Aidha, amesema kwasasa kuna zaidi ya watumiaji milioni 35.75 wa huduma za fedha kupitia simu ikilinganishwa na watumiaji milioni 23.34 mwaka 2018, ambapo Serikali ya Tanzania imewekeza maelfu ya kilomita za Mkongo wa Taifa wa TEHAMA (NICTBB).

“Mkongo wa Taifa unaunganisha nchi zisizo na Bahari kupitia maeneo ya mpakani ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi wenye urefu wa KM 18,000 na ili kupata mitandao ya mawasiliano, Tanzania imeanzisha Timu ya Kukabiliana na Dharura ya Usalama wa Kompyuta (TZ- CERT) ili kuratibu matukio ya kimtandao ngazi ya kitaifa.” amesema Nape.

Katika kuhakikisha nchi nzima inaunganishwa katika mawasiliano, Tanzania imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF). Hadi sasa Mfuko umeweza kuunganisha vijiji 316vyenye wakazi 730,000 ambapo mfuko wa Mawasiliano kwa wote pia umeanzisha miradi mingine ikiwa ni pamoja na kuunganisha shule, vituo vya mawasiliano na miradi mingine mingi.

Uchaguzi wa baraza Kuu la ITU unatarajiwa kufanyika tarehe 3 Oktoba 2022, ambapo Tanzania na nchi zingine 16 zinawania nafasi 13 kuwakilisha bara la Afrika. Baraza hilo lina jumla ya wajumbe 48.

Waandamana kutaka uhalali watoe mimba
19 wafariki kwa kunywa Pombe yenye sumu