Dakika chache kabla ya kumkabidhi uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Dk. Jakaya Kikwete amemueleza matatizo na udhaifu wa wanachama na viongozi wake.

Dk. Kikwete amesema kuwa ingawa wanachama wa chama hicho wamekuwa mahili wakati wa uchaguzi, wamekuwa hawalipi ada ya uanachama wao hali inayokifanya chama hicho kuzorota kifedha wakati mwingine.

“Kwahiyo pamoja na uzuri wote, ujasiri na ushababi wa wana CCM katika kupigania chama chao wakati wa uchaguzi, hatulipi ada. Mheshimiwa mwenyekiti unaesubiri kuapishwa nakuachia hili,” alisema.

Alisema kuwa kwakuwa chama hicho kina wanachama zaidi ya milioni 8 wangelipa kodi ya shilingi 1200 ipasavyo wangeweza kukiinua chama hicho kiuchumi na kufanya kazi zake ipasavyo. Aliongeza kuwa wanachama wengi husubiri kulipiwa ada na wagombea wakati wa chaguzi mbalimbali.

Aidha, alimueleza Rais Magufuli kuwa moja kati ya udhaifu wa viongozi wa chama hicho ni kutotoka na kwenda kuzungumza na wananchi, kazi ambayo amedai inapaswa kuwa endelevu.

“Viongozi wetu wamekuwa wazito kutoka kwenda kwa wanachama na wananchi. Kama naongopa semeni hapa mbele ya mwenyekiti wetu mpya. Kazi ya chama ndani ya chama haifanyiki ipasavyo na ndani ya chama hawafanyi kazi ndani ya chama,” alisema.

“Jambo la kushangaza, wakati sisi viongozi wetu hawaendi kwa wananchi, watani zetu wanakwenda. Sasa kama chama tawala hatuendi kuongea na wananchi utabaki kuwa chama tawala, ipo siku utatoka,” alisema.

Alimtaka Rais Magufuli kutambua mapungufu hayo na kuhakikisha anayafanyia kazi kwa maslahi ya chama hicho tawala.

Roma: Siasa sio jambo la msimu kama kombe la dunia
JK: Haikuwa Rahisi kumshawishi Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM