Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Pablo Franco Martin amemkingia kifua Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi chake John Raphael Bocco, kufuatia kiwango duni alichokionesha kwenye mchezo wa jana Jumatatu (Januari 17), dhidi ya Mbeya City.

Simba SC ilipoteza mchezo huo kwa kukubali kufungwa bao 1-0, na kuangusha alama tatu za kwanza kwa msimu huu 2021/122.

Kocha Pablo amesema Bocco hakucheza vizuri, lakini haikuwa kusudi lake kufanya hivyo, bali ilitokea mambo kumuendea hovyo na kushindwa kuisaidia timu yake kwenye Uwanja wa ugenini.

“Inatokea tu mchezaji kuna wakati inakuwa hivyo, sio kusema Bocco hajui hapana, ni namna ya mchezo unavyokuwa na ushindani wake, unakuta pia mchezaji anajipanga kweli kweli kuhakikisha anafanya kile anachokitarajia akini ikitokea akakwama, inamuumiza hata yeye mwenyewe,”

“Bocco ni mchezaji mzuri na ndio maana ni nahodha na mimi nafahamu namna ambavyo anajisikia kutokana na msimu uliopita alivyofanya vizuri lakini kwa sasa hajafanya vile.” amesema Kocha Pablo.

Bao pekee na la ushindi kwa Mbeya City lilifungwa na Mshambuliaji Paul Nonga dakika ya 20.

Kwa matokeo hayo Simba SC inaendelea kuwa na alama 24 zinazoiweka nafasi ya pili, baada ya kucheza michezo 11, huku Mbeya City ikifikisha alama 19 na kukwea hadi nafasi ya tatu.

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 32, baada ya kushuka dimbani mara 12.

Rais Samia afanya uteuzi
Simba SC yaomba radhi