Shirikisho la soka duniani FIFA, limepangua mipango ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil Adenor Leonardo Bacchi “Tite” ya kukusudia kuchelewa kutangaza kikosi kitakachoendelea na jukumu la kusaka nafasi ya fainali za kombe la dunia mwishoni mwa mwezi huu.

Tite alikuwa na mipango ya kuchelewa kufanya hivyo kwa kusudio la kutaka kupisha michuano ya Olimpiki inayoendelea nchini Brazil ambapo kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23 cha nchi hiyo kinashiriki michuano hiyo.

FIFA wameliagiza shirikisho la soka nchini Brazil CBF, kuhakikisha kikosi kinatangazwa haraka iwezekanavyo ili majina ya wachezaji watakaoteuliwa yaweze kutumwa mjini Zurich kwa wakati.

Kanuni za FIFA huzitaka nchi wanachama kutaja vikosi vyao siku 15 kabla ya michezo ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia.

Kwa mantiki hiyo Tite anatarajiwa kutangaza kikosi baadae hii leo ama mapema hapo kesho.

Kocha huyo ambaye alikua mkuu wa benchi la ufundi la klabu ya Corinthians, alidhamiria kuchelewa kwa lengo la kuwafuatilia wachezaji vijana wanaendelea na jukumu la Olimpiki kwa sasa, ili kuona kama baadhi yao ataweza kuwajumuisha kikosini mwake.

Timu ya taifa ya Brazil, inatarajia kupambana na Ecuador pamoja na Colombia katika michezo ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

Michezo hiyo itakua ya kwanza kwa Tite mwenye umri wa miaka 55, kukaa katika benchi la ufundi la Brazil, mara baada ya kukabidhiwa mikoba iliyoachwa na Carlos Dunga, ambaye alitimuliwa kufuatia kushindwa kufikia malengo ya kufanya vyema wakati wa michuano ya Copa America iliyofanyika mwezi Juni mwaka huu.

Ujumbe Huu Umeshika Kasi Mitandaoni
Wimbo Mpya: Young Killer - Mtafutaji