Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa anaamini siku moja atakuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lowassa ameeleza kuwa katika kipindi hiki anajiandaa tena kuwania nafasi ya urais mwaka 2020 na ameweka imani yake kuwa atashinda uchaguzi huo.

“Niko fiti na morali yangu iko juu naiona kazi hiyo ndiyo kwanza imeanza. Najua kama Mungu amepanga nitakuwa Rais wa Tanzania na niko tayari kuanzia sasa na ninaamini tutashinda [2020] kama tulivyoshinda katika uchaguzi uliopita, Oktoba 25,” alisema.

Lowassa alielezea msimamo ambao unaonesha kufuata nyazo za mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amekuwa akigombea urais wa Zanzibar tangu mwaka 1995 na kufikisha awamu ya Tano mwaka jana.

Lowassa ambaye alihamia Chadema baada ya jina lake kukatwa katika kinyang’iro cha kugombea urais kupitia CCM, alieleza kuwa hatachoka kugombea urais hata mara tano huku akifananisha uamuzi wake huo na ule uliofanywa na wanasiasa wakongwe ambaye hatimaye walifanikiwa kuwa marais wa nchi zao.

“Sitakuwa kiongozi wa kwanza kuwania mara tano kwa sababu yupo rais mmoj wa Marekani aliyewahi kuwania zaidi ya mara nne na alifanikiwa kupata urais,” Lowassa alisema jana jijini Dar es Salaam alipotembelewa na wafanyabiashara wa soko la Kariakoo waliokuwa wanamuunga mkono kwenye kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.

Bila shaka, Lowassa alikuwa anamzungumzia rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln aliyeshinda uchaugzi wa urais mwaka 1860 baada ya kushindwa mara kadhaa sio tu kwenye nafasi ya urais lakini pia wakati mwingine kwenye nafasi zingine za uongozi alizowania.

Pamoja kuwa alipitia maisha ya kushindwa mara kadhaa kabla hajawa rais, Lincoln anatajwa kuwa moja kati ya marais bora wa Marekani waliowahi kutokea.

Kadhalika, Lowassa alimtaja rais wa Senegal kama mfano wa harakati za kuingia ikulu bila kukata tamaa alizozianzisha.”Mwingine ni rais wa Senegal, Abdoulaye Wade,” alisema.

Baba amng'ata mwana kama Paka akimfunza asiwe 'Shoga'
Serikali yaleta mnyoosho mpya wa 'Watoro Kazini'