Baada ya kuisaidia Tottenham Hotspurs kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri, huku akifunga mabao mawili dhidi ya Man Utd katika mchezo wa mzunguuko wa tatu wa ligi ya England mwanzoni mwa juma hili, mshambuliaji wa pembeni kutoka Brazil Lucas Rodrigues Moura da Silva (Lucas Moura), ametamba kuwa na matumaini ya kuisaidia klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London, na kumaliza ukame wa mataji uliotawala kwa miaka kumi.

Moura mwenye umri wa miaka 26, ametoa tambo hizo, kwa kuamini amekua chaguo sahihi la meneja wa Spurs Mauricio Pochettino, tangu alipoanza kumtumia kimamilifu msimu huu.

Mshambuliaji huyo amekua katika mipango ya meneja huyo kutoka Argentina, kufuatia Heung-Min Son kuwa katika majukumu ya kuitumikia timu ya taifa ya Korea Kusini katika michuano ya Asian Games inayoendelea nchini Indonesia.

Moura, ambaye alijiunga na Spurs akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain mwezi Januari, amesema: “Hakuna kitakacho shindikana msimu huu, uwepo wangu na wa wachezaji wengine utafanikisha hatua ya kuiwezesha Spurs kurejesha heshima ya kutwaa mataji.”

“Ni muda mrefu umepita katika historia ya klabu hii kuwa na furaha ya kutwaa mataji, lakini kwa msimu huu hatutatoka kapa.”

Kuhusu uwepo wake katika kikosi cha Spurs na kutumika kama mchezaji tegemeo, mshambuliaji huyo amesema: “Ninajihisi faraja kuwa sehemu ya wachezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha Spurs, nilitarajia nafasi hiyo tangu niliposajiliwa hapa mwezi Januari,”

“Sifanyi haya kwa makusudio yangu ubinafsi, bali ninatambua ushirikiano uliopo dhidi ya wachezaji wenzngu ndio chanzo cha kuanza vizuri msimu huu katika ligi ya England, dhumuni langu kubwa la kuwa hapa ni kuhakikisha klabu inafanya vizuri, na kwa hilo sina wasiwasi, tutafikia lengo mwishoni mwa msimu huu.”

Usajili wa Yaya Toure kizungumkuti
Lugola amaliza utata mwili uliosuswa mochwari