Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa nchini Tanzania hakuna ubanaji wa uhuru wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee.

Amesema kuwa jambo hilo linadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati yake ni vituo vitatu tu ndivyo vinavyomilikiwa na Serikali.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania inaongozwa na katiba na sheria za nchi ambazo zinatoa uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesema Majaliwa

Amesisitiza kuwa mwananchi yeyote atakayeenda kinyume na sheria, Serikali itamuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Aidha, amesema Serikali imeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na ule wa haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Sambamba na kusimamia haki hizo, Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wake katika kuiwezesha jamii kuishi salama kwa amani na utulivu kwa kuzingatia sheria za nchi.

Maadhimisho hayo ya siku ya Umoja wa Mataifa ambao umetimiza miaka 73 tangu uanzishwe yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.

Wengine ni Mratibu wa Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Alvaro Rodrigues pamoja na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

UNHCR yaitahadharisha Marekani isikiuke sheria za kimataifa
TOC yafafanua mipango ya kufuzu Olimpiki 2020

Comments

comments