Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa kati na wadogo wadogo wa Kariakoo ambapo amewataka wasikubali kutoa rushwa kwa chombo chochote.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inapiga vita vitendo vya rushwa, hivyo wakiona kuna mazingira ya rushwa watoe taarifa kwani rushwa ni adui wa haki.

Waziri Mkuu amekutana na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Anatouglo jijini Dar es Salaam. ambapo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepata mafanikio makubwa baada ya kupiga vita rushwa.

“Rushwa si sehemu ya mkakati wa Serikali, hivyo vita dhidi ya rushwa lazima iendelezwe na watu wote. Mafanikio tuliyoyapata ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za afya ni matokeo ya kupiga vita rushwa.”amesema Majaliwa

Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wawe na tabia ya kuwatembelea wafanyabiashara kwenye maeneo yao na kusikiliza kero zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha, Majaliwa amesema kuwa Serikali imepanga mpango wa kubadilisha utaratibu wa kufanya biashara katika eneo la Kariakoo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 kama yalivyo masoko makubwa duniani.

Hata hivyo, katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu kuziunganisha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). ambapo amesema kuwa TFDA na TBS zinafanya kazi ambazo zinafanana hivyo Mawaziri hao wakutane na wafanye mapitio ya kazi za mamlaka hizo na waandae muswada kuunganisha mamlaka hizo na kuuwasilisha bungeni.

Mbowe, Matiko washinda Rufaa kuhusu dhamana
CCM Njombe yawatoa hofu wananchi kuhusu mauaji ya watoto

Comments

comments