Jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watuhumiwa wawili wa makosa mbalimbali, likiwemo tukio  la Mtoto kumuua baba yake mzazi kwa ngumi na tukio la kupatikana na Pembe ya ndovu yenye thamani ya Tshs 34,635,000/=.

Inaelezwa Mnamo tarehe 31/05/2020 majira ya saa 12 alfajiri huko Gairo, Issaya Lameck (41), Fundi Muwashi, mkazi wa kitongoji cha Manyani, aliuawa kwa kupigwa ngumi usoni na kukanyagwa sehemu mbalimbali za mwili wake na mtoto wake aitwae Yohana Issaya, Miaka 17.

Akielezea tukio hilo kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Wilbroad Mutafungwa amesema Awali siku ya tarehe 30/05/2020 majira ya 12 jioni, marehemu alirudi nyumbani kwake akiwa amelewa ndipo ulipozuka ugomvi na mtoto wake huyo ambaye alimpiga ngumi baba yake sehemu za usoni na kudondoka chini kisha kuendelea kumkanyaga sehemu za tumboni, hali iliyopelekea kupata maumivu makali mwilini mwake.

Baada ya tukio hilo ndugu wa marehemu waliingilia ugomvi huo lakini hawakuweza kumpatia msaada wa kimatibabu kutokana na hali ya ulevi aliokuwa nao wakati wa tukio hilo na marehemu kudai kuwa hajaumia na ilipofika siku ya 31/05/2020 majira ya saa 12 alfajiri alizidiwa na kufariki dunia.

Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa taratibu za mazishi.Mtuhumiwa amekamatwa na anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake la mauaji.

Katika tukio jingine Mnamo tarehe 1/6/2020 majira ya  saa 01 asubuhi huko Kilosa, askari Polisi kwa kushirikiana na askari wa Wanyama Pori wa hifadhi ya Mikumi wakiwa doria na misako  walipokea taarifa za kuwepo kwa mtu akiwa na nyara za serikali.

Walipofuatilia walifanikiwa kumkamata Nuru Mohamed (35), mkulima, mkazi wa Kasiki akiwa nyumbani kwake na baada ya kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake alikutwa akiwa na Pembe moja ya Ndovu yenye uzito wa kg 7.5 na thamani ya Tshs 34,635,000/= ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa sadalusi kisha kufichwa katika uvungu wa kitanda chake. 

Imeelezwa kuwa mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na hatua za kumfikisha mahakamani zinafuata.

Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia za ulevi uliopitiliza ambao hupelekea matukio mabaya kama ya mauaji na wote wanaojihusisha na shughuli za ujangili kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dora limejipanga kuhakikisha matukio yote yanadhibitiwa na watuhumiwa wanatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani.

Infantino: Thuram, Sancho, Hakim hawapaswi kuadhibiwa
Ahadi ya JPM yaanza kutekelezwa, miezi 13 ya kupata maji Kyaka-Bunazi.