Mkuu wa Idara ya Habari Mawasiliano Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene amesema kuwa mwanachama wa Chama hicho, Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema ametekwa na watu wasiojulikana akiwa ofisini kwake Vwawa-Mbozi

Amesema kuwa magari mawili yalivamia ofisini kwake, wakashuka watu wanne, naye alipiga kelele Wananchi wakajitokeza lakini Watu hao waliwatisha kwa bastola.

“Imedaiwa kuwa baada ya muda mfupi kulisikika purukushani, watu hao wakijaribu kumkamata Mdude huku wakimpiga na yeye akipiga kelele za kupinga kitendo hicho na kuomba msaada” amesema Makene

Amesema tayari Chadema kupitia kwa viongozi wa Chama katika eneo husika na Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga, kimevitaarifu vyombo vya dola kuanza kutoa taarifa ya tukio hilo lenye mazingira ya utekaji pia kutaka kujua kama kuna askari waliopewa kazi ya kwenda kumkamata Mdude.

Kufuatia taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amesema hana taarifa kuhusu tukio la kutekwa kwa mwanachama huyo.

Kamanda Kyando amesema taarifa ya kukamatwa kijana huyo hajazipata na kwamba hakuna milio ya risasi iliyosikika katika maeneo hayo. Amesema ataendelea kufuatilia kwa kina zaidi juu ya taarifa hizo na kwamba baadaye leo huenda ukweli ukajulikana.

“Mimi ni mkazi wa eneo linalodaiwa kuwa risasi zimepigwa lakini sijasikia na kama unavyojua mji wa Vwawa ni mdogo ambao zikipigwa risasi lazima utasikia,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga amesema: “Kweli Mdude ametekwa na watu waliokuwa kwenye magari mawili, Nissan Patrol na Landcruiser na walifika ofisini kwake mjini Vwawa-Mbozi. Na hadi sasa  sijui yuko wapi.”

Amesema tukio hilo limetokea jana saa 12 jioni na baada ya tukio hilo amewasiliana na Kamanda Kyando lakini amejibiwa kwamba hana taarifa hizo na wao (polisi) hawajamkamata.

“Nimezungumza na RPC ameniambia hawajui na siyo wao waliomkamata. Lakini pia nimetoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemas Mwengela kuhusiana na tukio la kutekwa kwa Mdude,” amesema Haonga.

Amesema mbali na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola lakini pia ametoa taarifa kwa uongozi wa juu wa Chadema na wanaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya tukio hilo ili kujua Mdude amechukuliwa na watu gani na amepelekwa wapi.

Basi la Kilimanjaro Express lapata ajali Tanga
Katibu wa Uenezi CCM Njombe acharuka, ' Msiitegemee Serikali'

Comments

comments