Kocha Mkuu wa Ndanda FC Meja Mstaafu wa Jeshi La Wananchi Tanzania (JWTZ) Abdul Mingange, amethibitisha kukamilisha maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa Robo Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) dhidi ya Sahare All Stars.

Mchezo huo watatu wa Robo Fainali msimu huu 2019/20, utachezwa kuanzia mishale ya saa kumi jioni kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Mingange amesema baada ya kuwasili mjini Tanga kikosi chake kilifanya maandalizi ya mwisho, na atapambana ili kuhakikisha anapata ushindi dhidi ya Sahare All Stars ambao watakua nyumbani.

Hata hivyo kocha huyo mzawa ametoa angalizo la upinzani kwa kusema anatarajia mpambano kuwa na vuta ni kuvute, kutokana na timu za madaraja ya chini zinapokutana na timu za ligi kuu huwa zinakamia katika muda wote wa dakia 90.

“Timu za madaraja ya chini zikikutana na za ligi kuu huwa zinakamia, hivyo tumejipanga kwa namna yoyote kukabiliana na hilo,kwani natambua imetusoma wakati tunacheza mechi za ligi kuu.

“Awamu hii tunapambana kadri tuwezavyo kuhakikisha tunavuka hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA,baada ya kuishia robo fainali huko nyuma,” amesema Meja Mingange.

Amesema anaamini Sahare All Stars itawapa ushindani mkubwa kwani kundi kubwa la wachezaji wao linataka kutumia fursa hiyo kujitafutia soko.

“Ukiachana na hilo kuna wachezaji ambao watataka kuonekana na Ndanda FC ili kupata bahati ya kucheza ligi kuu kwani naamini hatushuki,” amesema Mingange.

Tayari Young Africans na Namungo FC zimeshakata tiketi ya kucheza Nusu Fainali ya michuano ya Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC), kufuatia kushinda michezo yao ya jana Jumanne.

Young Africans waliifnga Kagera Sugar mabao mawili kwa moja Uwanja wa Taifa Dar es salaam, huku Namungo FC wakicheza nyumbani Majaliwa Stadium waliichabanga Alliance FC mabao mawili kwa sifuri.

Mchezo mwingine wa Robo Fainali utachezwa leo Jumatano kuanzia mishele ya saa moja jioni Uwanja wa Taifa Dar es salaam, kati ya Mabingwa Watetezi Azam FC dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC.

Marekani yanunua dawa yote ya corona iliyothibitishwa, bei ya dozi yawekwa wazi
Mwenyekiti wa CCM Ubaruku auawa kwa shoka kitandani