Kiungo mshambuliaji kutoka Ghana, Bernard Morrison amefunguliwa milango ya kurudi kundini, lakini kwa sharti la kuomba radhi wachezaji wenzake, benchi la ufundi, mashabiki, wanachama pamoja na viongozi na wadhamini wa klabu hiyo.

Morrison aligomea safari ya kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya mwadui FC, huku akizima simu, jambo ambalo lilizua taharuki kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa Young Africans.

Kiungo huyo pia alihusishwa na tetesi za kurubuniwa na baadhi ya wadau wa soka nchini kwa kumtaka aikache Young Africans, katika kipindi hiki, kwa madai ya mkataba wake wa miezi sita na klabu hiyo kufikia kikomo.

Fursa ya kurejea kundini kwa Morrison imetolewa na kocha mkuu wa Young Africans Luc Eymael, ambapo amesema mchezaji huyo atakuwa na nafasi hiyo ya kipekee pindi timu itakaporejea Dar es salaam, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesisitiza kwamba, Morrison pamoja na mchezaji yoyote wa Young Africans lazima ajue kwamba kila kitu anachokifanya ni kama timu na huku akionya kuwa hakuna mchezaji nyota asiyepata msaada uwanjani kutoka kwa wenzake.

Amesema amezungumza na mchezaji huyo kwa dakika 50 na kusema kiungo huyo amebaini kosa lake ambalo anajutia, huku akiwalaumu baadhi ya mawakala kwa tamaa na kushawishi vibaya wachezaji.

Eymael amesema Morrison amegundua njama hizo na kukiri kukosea na ataomba radhi mbale ya wachezaji ili kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC ambao utatoa picha halisi ya timu ipi itashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Mimi sikuwepo, nimekutana mambo mengi ambayo si ya kawaida ndani ya klabu, kama kocha mkuu ni jukumu langu kutatua na kuiweka sawa timu.

Morisson ni moja ya tatizo hilo na hakuweza kusafiri kwenda Shinyanga, nilitaka kujua kuna tatizo gani, lakini muda haukutosha na kuamua kuondoka na (David) Molinga,” alisema Eymael.

Amemtaka Morrison kujua kuwa hakuna mchezaji nyota duniani anayecheza mpira peke yake uwanjani bila msaada wa wengine, “hata ukiwachukua kina Cristiano Ronaldo wawili, Messi wawili na Sergio Ramos wawili wacheze dhidi ya wachezaji 11, lazima watafungwa. Timu ni mchango wa watu wengi.

“Najua Morrison kwa sasa ndiye mchezaji nyota wa Yanga, hilo halina ubishi, lakini lazima ajue kuwa umaarufu wake unatokana na msaada au ushirikiano na wachezaji wengine hilo ni jambo muhimu kujua, Yanga ni timu na wala si ya mchezaji mmoja pekee.”

Callum Hudson-Odoi akwepa kifungo
JPM atahadharisha kampeni za matusi, awashukuru wapinzani