Siku chache baada ya kuenea kwa taarifa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ana mpango wa kukihama chama hicho kufuatia mgogoro wa uongozi unaoendelea, chama hicho kimetoa msimamo wake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui amekanusha taarifa hizo na kueleza kuwa taarifa hizo ni miongoni mwa jitihada za kutaka kuwakatisha tamaa.

“Hivi unafikiria Katibu Mkuu anaweza kuhama chama katika mazingira rahisi kiasi hicho? Hiki chama amekipigania vya kutosha wataondoka wao,” Mazrui anakaririwa.

Chama hicho kimekuwa na mgogoro mkubwa wa uongozi baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kubadili msimamo wake wa kujiuzulu Uenyekiti wa chama hicho na baadae kutambuliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa.

Chama hicho kimegawanyika kutokana na mgogoro huo, ambapo kwa kiasi kikubwa upande wa Zanzibar unamuunga mkono Maalim Seif na upande wa Bara wanamuunga mkono Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine, Mazrui alisema kuwa chama hicho kinaendelea na jitihada za kupigania kile wanachodai kupokonywa ushindi wa Urais wa Zanzibar, huku akisisitiza kuwa suala hilo litamalizika vizuri kwa busara.

“Suala la madai ya ushindi wa uchaguzi linakwenda vizuri, na naamini hatima yake itapatikana kwa busara, ni vema wana CUF kuwa na subira,” alisema.

Wananchi watakiwa kuhifadhi fedha zao benki
Video: Kinana, Nape kung'oka CCM, Joto la Magufuli latua...