Benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar chini ya Kocha Mkuu Salum Shaban Mayanga limetoa ufafanuzi wa kuwatema baadhi ya Wachezaji waliokuwa nao Msimu uliopita, na kufanya usajili wa Wachezaji wapya kuelekea Msimu mpya wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC.

Kocha Msaidizi Awadh Juma amesema wamelazimika kuwaacha baadhi ya wachezaji na kuwasajili wengine ili kuleta chachu mpya ya ushindani ndani na nje ya kikosi chao, kuelekea msimu mpya wa 2022/23.

Awadh ambaye aliwahi kuitumikia Mtibwa Sugar kama Mchezaji amesema, maamuzi hayo yamekuja kufuatia upembuzi yakinifu wa kiufundi uliofanywa na Benchi lao la Ufundi na kubaini kulikua na haja ya kufanya maamuzi hayo magumu.

“Mwaka jana tulikua na namba kubwa zaidi ya Wachezaji, mwaka huu tumepunguza wachezaji 20, tumepandisha Wachezaji kutoka kwenye kikosi chetu cha U20, pia tumesajilia Wachezaji wengine.”

“Maamuzi haya ni kutaka kuleta chachu mpya ya ushindani ndani na nje ya kikosi chetu, kama unavyojua hatukufanya vizuri msimu uliopita na hata msimu uliotangulia nao hatukufanya vizuri, kwa hiyo maamuzi haya yalikua ya lazima kufanyika.”

“Tunaamini Mabadiliko tulioyafanya yanakwenda kuleta ushindani mkubwa baina ya Wachezaji wenyewe na timu tutakazokutana nazo msimu ujao, kwani Wachezaji tuliowasajili na wale tuliowapandisha wana uwezo mkubwa wa kupambana.”

“Imani yetu ni kutaka kuiona Mtibwa Sugar inarudi katikla hadhi yake ya kupambana kama miaka ya nyuma, tunaamini hilo linawezekana, na hakuna muda mwingine zaidi ya Msimu ujao ambapo kuna jambo tunakwenda kulifanya katika mashindano tutakayoshiriki.” amesema Awadh Juma

Mtibwa Sugar ilikua na Msimu mbaya na kufikia hatua ya kucheza michezo ya hatua ya mtoano (Play Off) dhidi ya Tanzania Prisons na kuishinda klabu hiyo ya Mkoani Mbeya.

Augustine Okrah achimba mkwara Ligi Kuu, ASFC
Uhuru adaiwa kuwaasi wandani wake wa zamani