Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amerejesha sakata la korosho zinazolimwa Lindi na Mtwara, ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akidai kuwa tasnia ya zao hilo imevurugwa na watendaji wachache wa Serikali.

Akizungumza jana wakati wa kutoa mchango wake bungeni, Nape alieleza kuwa walioenda kutekeleza dhamira njema ya Rais John Magufuli hawakufanya kazi yao ipasavyo na badala ya kuboresha tasnia walivuruga tasnia hiyo.

“Kulikuwa na nia njema ya Serikali. Mheshimiwa Rais aliweka nia njema. Walioenda kuitekeleza nia njema ya Rais wameenda kukoroga na kuua sekta ya korosho. Hivi tunavyoongea, bahati mbaya zoezi lilikumbwa na dhuruma, lilikumbwa na rushwa, lilikumbwa na ubabaishaji mwingi sana na uongo mwingi sana,” alisema.

“Hivi tunavyoongea mheshimiwa Spika, jimbo la Mtama peke yake, kwenye vyama vya msingi 11, wakulima ambao wana korosho chini ya tani 1,500 ambao wamehakikiwa mashamba yao zaidi ya 1,281 kwa miezi nane toka korosho yao ichukuliwe hawajapata senti 5,” aliongeza.

Alisema kutokana na hatua hiyo, wakulima wameshindwa kuanza kulima mashamba yao wakati ambapo msimu mwingine umeshaanza kwani hawana fedha za kuwawezesha.

Nape alipendekeza kuwa Sheria ya Korosho iliyofanyiwa marekebisho irejeshwe bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho tena kwani baadhi ya vipengele vilivyoondolewa ndivyo vilivyosababisha matatizo makubwa ya sheria nzima.

Aidha, Mbunge huyo wa Mtama alipendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenda kukagua zoezi lilivyofanyika na kuwasilisha ripoti bungeni.

Alisema watu walioshiriki kutekeleza zoezi hilo ambao walilivuruga wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuharibu sekta ya korosho kwani korosho zilizopo haziwezi kuwa na ubora unaotakiwa baada ya kukaa ghalani zaidi ya miezi sita.

Alifafanua kuwa watu hao wanapaswa kuchukuliwa hatua mmoja mmoja badala ya kuiingiza Serikali yote kwenye lawama zilizosababishwa na utendaji mbovu wa watu wachache.

Video: Masele akalishwa kiti moto Dodoma, Korosho zawa moto bungeni
Tibaijuka afafanua kauli ya ‘milioni 10 ni pesa ya mboga’, sakata la Escrow

Comments

comments