Saa chache baada ya kuthibitika hatakuwa sehemu ya Kikosi cha Simba SC kwa msimu ujao 2023/24, Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Augustin Okrah amefunguka ya moyoni.

Okrah anaondoka Simba SC baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa msimu mmoja ambao ulikuwa na bahati mbaya kwake, kwani aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara, hali ambayo ilimfanya kushindwa kuonyesha uwezo wake kikamilifu.

Okrah amefunguka kupitia kurasa zake za Mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno mazito ambayo yataendelea kuacha alama katika maisha yake ya soka na kwa Mashabiki wa Simba SC ambao walimpokea kwa shangwe aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu huko Msimbazi akitokea Bechem United ya kwao Ghana.

Okrah ameandika: Maisha yetu ya kitaaluma yamejaa watu wanaokuja na kuondoka, watu tunaowakumbuka, na wale wanaofifia. Ninapoendelea kutoka hapa, ninawaweka kila mmoja wenu katika kumbukumbu, shukrani kwa muda wote tuliotumia pamoja. Nawakumbuka nyote, asante kwa yote mliyonipa, kazi yetu ituletee pamoja tena, asante Simba SC, asanteni mashabiki wa Simba SC, mashabiki wangu na asante Tanzania.

Mapama leo Jumatatu (Juni 05) Simba SC ilithibitisha kuachana na Okrah katika vyanzo vyake vya habari, huku ikimtakia kila la kheri katika maisha yake mapya baada ya kuondoka klabuni hapo.

Kupitia vyanzo vya habari za Simba SC taarifa ya kuondoka kwa Kiungo huyo imeandikwa: Baada ya kuwa kwenye kikosi chetu kwa msimu mmoja, Augustine Okrah hatakuwa sehemu ya timu yetu ya msimu ujao. #WenyeNchi #NguvuMoja

Miili 180 isiyotambuliwa yazikwa na wasamaria
Kocha Nabi atangaza kiama Ligi Kuu, ASFC