Matumaini ya kubaki kwa kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba kwenye klabu ya Manchester United yamefufuka, kufuatia Meneja wa klabu hiyo Ole Gunnar Solskjaer kudhihirisha hitaji la huduma ya mchezaji huyo.

Kabla ya kuibuka kwa janga la virusi vya Corona ilikuwa inafahamika kuwa kiungo huyo angeondoka Old Trafford baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa Mfaransa huyo angetimukia Real Madrid au Juventus FC, lakini anaonekana kufurahia maisha ndani ya Manchester United.

Licha ya tetesi hizo, tangu Pogba arejee uwanjani akitokea kwenye majeruhi ya muda mrefu ametengeneza muunganiko mzuri na kiungo mshambuliaji kutoka Ureno Bruno Fernandes, na kufanikisha uimara wa kikosi cha Manchester United.

Mkataba wa Pogba mwenye umri wa miaka 27, utafikia kikomo mwishoni mwa mwaka 2021, lakini uongozi wa klabu hiyo una kipengele cha kumuongezea mkataba mpya.

Endapo Manchester United watafanikiwa kumbakiza Pogba, kocha Ole Gunnar Solskjaer atakuwa ameingia mkataba na viungo wake wote, ambapo juma lililopita alifanikiwa kumsainisha mkataba Mserbia Nemanja Matic na Scott McTominay.

“Ili kuwa klabu kubwa lazima tuwe na wachezaji wakubwa, tuna matumaini tunaweza kumshawishi kiungo huyo”. Alisema Solskjaer.

“Paul tangu aliporudi kutokea kwenye majeruhi anaonekana kuimarika siku hadi siku, anafurahia kucheza nasi, gonja tuone tutakapopelekwa na hili” aliongeza.

Kenya yafuata nyayo za Tanzania, yafuta karantini kwa watalii, wageni
Prof. Makubi: Kutoa huduma za afya za uhakika ni jukumu letu